Wednesday, November 23, 2005

Tunapinga na kupinga...

unajiita sauti ya wanyonge,
lakini muda pekee unapotoa sauti yako
ni pale unapopinga walichosema wenzio....
Bahati dube, wimbo: mchezo wangu (my game).

Nimekumbuka wimbo wangu kipenzi toka kwa gwiji la reggae dube, sijui kama wimbo huu uliwahi kupata tuzo, labda ni muendelezo wa hadithi za muziki wa kitumwa wa kisasa zilizoanziswa na msangi, ndesanjo jeff na nkya kudakia.
Wanablogu tunataka kuingia kwenye hali hii, tunajifanya kwamba ni sauti za wanyonge lakini kumbe tunachofanya ni kupinga wanachofanya wenzetu, sijui tuna wivu sana kwa kukosa maendeleleo kama wao ama ni kutaka kuwa juu ya watu wote!
Wenzetu wa kizazi kipya, kisichojua tofauti ya uhuru na utumwa, Utamaduni na hadithi, Chao na cha wenzao, mwanzo na mwisho.... na kuuita muziki wa kizazi kipya, kama tulivyo tumedakia na kuupigia kelele wakati hata siku moja hatujawahi kuwaonyesha mathalani kuwafundisha muziki wetu uko vipi, Sembuse kuwapa nafasi ya kutatua matatizo yao kupitia muziki WETU, tunatarajia vijana kuupenda muziki wetu na kuacha mingine inayowafikia kwa urahisi kuliko yetu.
Tuliangalia Mashirika ya umma yakiteketea, bila kufanya juhudi za kuyaokoa,siyo kulia tu ila kwa kujitolea hata damu kuyatetea kama mashahidi wa uganda walivyomtetea yesu kwa kabaka, tuliona ni sawa tu kwanza hayatupunguzii kitu na wala hayatuhusu!, ukweli ukaonekana kwamba tunahitaji yawepo kwani huduma zake zilihitajika sana, serikali ikaona njia pekee ni kuyabinafsisha lakini wakaanza sasa yanafanya uzalishaji kwa ufanisi wanablogu tunalia nchi imeuzwa! labda kati ya aliyeiua na anayeiuza ili ifufuliwe, wapili ni mbaya zaidi.
Serikali kivuli nayo iko kama wanablogu, wanaingia bungeni bila mipango, halafu ni mabingwa wa kukataa, ili wawape lawama serikali ikishindwa kwenye mipango yake. tunakuwa mabingwa wa kuchambua mipango ya wengine wakati hatuna yetu, Ila tunamawazo yanayopinga maamuzi ya wengine ingawa nayo pia tunayapanga tukiwa usingizini bila kuwashirikisha wanaolengwa na mipango hiyo. Sijui kama tukifanya sensa leo ya mambo yanayoandikwa kwenye blogu, mangapi yatakuwa sio mawazo binafsi ya mwanablogu aliyeyaandika? tukiendeleza sensa hii na kuangalia ukubalikaji wa hoja za blogu, sijui kama kutakuwa na hoja zao ila tu zetu hazipewi nafasi kwa sababu hatuna dola ya kuzisimamia. katika pitapita yangu kwenye vibaraza vingi nimeyaona haya, kila mahali wanamambo wanayoyapenda, ila hakuna kibaraza kinacholengana ma mawazo ya serikali!
Mwanamapinduzi Walter Rodney alianza kuishinda hali hii, kwenye mafundisho yake aliyaita "grounding with my brothers" aliwakusanya vijana na wanamapinduzi kisha kujadiliana nao, hii iliamsha ari yao ya mapinduzi na kumfanya rodney awe chakula cha risasi.
tuangalie sisi tufanye nini.

Wednesday, October 12, 2005

Makosa na usahaulifu.

Barua niliyomwandikia ndugu yangu nkya, sijui kam inaukweli ndani yake au inaweza kutumika kuombea PHd kwenye fani ya siasa.
Ndugu Hilo ndilo kosa la ANC naona liko kama kosa la Nyerere, yeye hakuamini kama ujamaa unaweza kuanguka, ilikuwa ni dhambi kama kufikiria kuwa papa. Alijenga mashirika ya umma bila kuwapa umiliki wananchi hivyo ujamaa ulipoanguka na hayo mashirika yalishindwa kuendeshwa na wananchi, sasa wakipewa wazungu kuyaendesha tunapiga kelele bila kutafuta chanzo, angalia wachina naona mao alijuwa hiki kitu akaandaa watu wake ili kuwa tayari kumiliki uchumi iwapo ukomunisti ungeanguka ndiyo maana wachina hawanashida na mwekezaji toka ulaya.Kila mchina ana uwezo wa kutengeneza kitu ambacho sisi tunatumia dola nyingi kuviagiza. Sijui fani yako, lakini naona kama sio technolojia ya chuma uchumi wa ulaya usingekuwa hapo ilipo sasa, wameweza kutengeneza vyombo vya usafirishaji, mitambo na pia vifaa vya kilimo vilivyowapatia maendeleo ya haraka. Sijui kama wangengoja wa-kushi wawatengenezee hivyo vifaa wangekuwa wapi sasa?. Sina takwimu sahihi lakini naona kama technolojia ya chuma hapa Tanzania haithaminiwi ndio maana tunaingia karne ya 21 bado tunatumia jembe la mkono!. Marekani iliendelea kwa kuwafanya waafrika watumwa wao kwenye mashamba na migodi, hilo sisi hatuliwezi, lakini tunao ng'ombe wengi wenye nguvu kama nyati kwa nini tusiwatumie kukuza kilimo? Ukinichagua mimi nitaleta maendeleo bila wananchi kujifunga mkanda, ghafla mahitaji yatajaa madukani, na pesa mifukoni hawaongelei, ukweli ni havitakuwa vya waliowapigia kura! Angalia ikapa hapo, huna haja ya kuwasha gari kwenda kazini, unauhakika wa kupanda treni au kama ni mwoga 'Golden arrow' ipo. Nini maana yake 1. Unakuwa umetunza mazingira kwa kutotengeneza moshi mchafu kuliko ukoma. 2. Umepunguza mafuta ambayo serikali hutumia mamillioni ya pesa za kigeni kuyaagiza baada ya kuhudumia wakulima na sekta nyingine zenye umuhimu. 3. Badala ya kuendesha gari ukiwa peke yako na kuleta msongamano mjini, utaupunguza kwa kutumiausafiri wa jumuiya- ambao ni nafuu zaidi kwa gharama.
Hayo ndiyo maoni yangu. Mjadala uko wazi kuchangia.

Wednesday, October 05, 2005

Samahani

Nimejaribu kualika watu pasipo na viti, samahani nilisahau, nafasi za watu kukaa. Walikuja wengi sana wakakuta hakuna nafasi ya kukaa hata mtu mmoja, sijui kama waliondoka kimyakimya kama mchungaji anaposisitiza watu wachangie sadaka nyingi zaidi au walitukana kama siku yanga ilipofungwa na simba.
Unajua kila kitu kina aina yake, kama vile wengine huandaa tafrija ndipo waalike watu kusheherekea kwa kunywa na kula lakini wengi hualika watu kuja kusaidia kuandaa tafrija hata kama haiwahusu au haina ulazima kwao wanatakiwa "kuchangia" ili ifanikiwe. Samahani hivi mimi ninaonekana niko kwenye kundi lipi?
Habari huandikwa na mwandishi wa habari lakini mimi sio mwandishi wa habari wa kuandikia watu, nataka watu waniandikie mimi nizisome habari zao, mko tayari kuniandikia bila malipo? Je watu hupenda kusoma kila habari iliyopo, sijui kama ukimwanbia Rasta afrika siyo kwao atakusadiki, labda ukitumia njia nyingine ambayo sijawahi kuisikia .
Habari zipo nyingine ni nzuri na nyingine ni mbovu nani anajua habari iliyo nzuri kila wakati, kama ni hivyo waandishi wasingekuwa wanazeeka na kujiuzulu kila siku au kufukuzwa kazi kwa ufanisi mbovu.Sio kama sikubaliani na uwapo wao, ila nahitaji kuwa na busara zaidi ya ile ipatikanayo toka kwa mmoja mmoja.
Kaa tuongee nilikuta nyumba ya wageni moja pale livingstone nchini zambia inaitwa tulye tonje nikaambiwa maana yake ni kaa tuongee, sijui kama itakuwa na uhusiano na hii kaa tuongee, hapa panaendeleza na hatufanyi mambo ambayo yatamdhuru mtu, sikumbuki kilichokuwa kinafanyika tulye tonje, maana nilifika usiku na mchovu wa safari hivyo nilifurahia kupata kitanda kama nimefika safari yangu.
Karibuni tukae tuongee, kila mmoja ashiriki katika maongezi haya tupate kilicho kweli hata kama kitawauma wengi na wachache wengine wajue kwamba wamekalia misumari na wasiponyanyuka haraka itawachoma washindwe kukaa kesho kama kesho huwa inafika.

Wednesday, September 28, 2005

Karibuni

Kaa tuzumze,
tuongee mambo mazuri,
tuelewane kwa maongezi,
pesa za kidunia zisituingilie,
wahenga nawaalika,
kwa heri na busara,
shari ikae mbali,
hata wanyonge wajongee,
walio mbali watusikie,
wakaribu watuone,
wasiojua uzuri wa tausi,
hawajui thamani yake,
tupendao usikivu,
twajua busara zake,
kila mmoja anaijua,
hata kama hajaipata,
siwezi kuitaja,
msaada naomba,
niweze ipa jina,
na wote waipate....