Friday, September 15, 2006

Ya Mugabe yamekemewa haya jee?

Nadhani ni wachache sana wanaojua kisiwa kinachoitwa chagos, kisiwa hiki kipo karibu na Tanzania kwenye bahari ya hindi na zaidi vipo karibu na visiwa vya mauritius. na wakazi wake ni waafrika weusi na matabaka mengine.
Kumbuka Ulimwengu wa Magharibi ukiongozwa na uingereza, Australia na Marekani wanavyompigia kelele na vitimbi vya kila aina shujaa wetu Bob Mugabe kwa kuwanyang'anya/ kuwapunguzia ardhi wazungu wachache pale Zimbabwe waliokuwa wamejilimbikizia ardhi huku weusi wengi wakiwa hawana ardhi hata za kujenga vibanda vya kuishi na familia zao.
Nimekuta katika jarida la New African toleo la Agosti/september 2006 Habari inayosikitisha na kuwaumbua hao kuwa wanachotaka Zimbabwe sio demokrasia wanayoisemwa ila kuna jingine lililojificha. Katika kipindi cha miaka ya 1965, na 1973 wakazi zaidi ya 2,000 wenyeji wa visiwa hivyo walifukuzwa toka kwenye visiwa hivyo na Uingereza na Marekani wakihamishiwa uhamishoni kwenye visiwa vya mauritius na shelisheli ili visiwa vyao vitumike kama vituo vya kijeshi vya Uingereza na Marekani na pia kwa utalii.
Wenyeji wa visiwa vya Chagos hawakukubaliana na uamuzi huo wakaendesha kampeni ,toka siku hizo mpaka leo bado wanaendelea, katika kesi iliyohukumiwa na mahakama kuu ya uingereza na mheshimiwa jaji Cresswell na Jaji Hooper kuwa uamuzi wa kuwafukuza haukuwa na busara na unachukiza wao, serikali ya Uingereza wanaukataa na kung'ang'ania kukata rufaa juu ya hukumu hiyo huku wakishinikizwa na rafiki zao Marekani kwa kuhofia usalama iwapo wa-chago watarejea kwenye ardhi yao ya asili.
Najaribu kufananisha hizi hali mbili; chagos na zimbabwe bila kupata jibu, ila nimeona kuwa hii ni vita nyingine ya kukomboa sehemu nyingine ya bara la afrika iliyosahaulika na ambayo hakuna anyeitangaza.