Wakati viongozi wa Afrika wanakutana na wenzao wa Uchina huko Beijing, China kuna mikutano mingine ya chini chini inaendelea baina ya viongozi wa nchi za kiafrika wanaohudhuria Mkutano huo mkubwa unaotarajiwa kulipatia manufaa makubwa sana bara la Afrika.
Uchina huwa haiamrishwi na Marekani na rafiki zake washirikiane na nani, hivyo maadui wakubwa wa jamii ya Marekani nao pia watahudhuria Mkutano huo mkubwa ambavyo Vyombo vya Habari(uongo!) wameanza kuutilia shaka bila ya kuwa na shaka na mambo yao wenyewe. Viongozi wa Afrika walioalikwa yumo kinara wa Afrika Raisi Bob Mugabe wa Zimbabwe aliye kwenye orodha kuu ya maadui wa magharibi, pamoja na Raisi wa Sudani Bwana Al-Bashir ambaye anasahau uafrika wake na kubariki kuangamizwa wenzake wa jimbo la Durfur kwa Sababu wao ni weusi zaidi yao! Na nywele zao ni ngumu sana!
Bila shaka, lazima Raisi wetu Mhe. J Kikwete na wenzake wengine watapata wasaha wa kukutana na Bw. Al-Bashir, na kufanya mazungumzo yaliyo au yasiyo rasmi. Ingawa kuna mambo mengi sana ya kuongelea ikiwamo ruhusa ya Tanzania kutumia maji ya Ziwa Nyanza! kukaribisha wawekezaji toka Sudan, uhusiano baina ya nchi hizi mbili. Ila bila kuongelea na ikibidi kukemea tabia au kusudi la Bw. Al-Bashir la kufumbia macho mauaji ya Durfur atakuwa hajawatendea haki watanzania na waafrika wote kwa ujumla, pia atakuwa hajatekeleza kipengele cha ilani yake ya uchaguzi aliyokuwa ameikariri kuliko misahafu kipindi cha kampeni cha kushughulikia migogoro ya jirani zetu.
Sitegemei kama kuna Mtanzania anayeunga mkono mauuaji hayo yanayoendelea kwa kasi sana, huku serikali ya sudan ikitajwa kuliimarisha jeshi la wauaji kwa kuwapatia silaha na kuzuia jeshi la nje kuingilia kati mauaji hayo.
Hivyohivyo, ingawa China ametuita kutupatia msaada naye inabidi aambiwe kwamba soko lake la silaha la Sudani linatuumiza sana kuliko hiyo misaada anayotaka kutupatia hivyo aache kuwauzia silaha wasudani na kwanza aingilie hayo mauaji ya Durfur na kuhakikisha yanakoma la siyo hiyo misaada yake haitakuwa na maana kwetu na itatuchefua zaidi kuona waafrika wanazidi kuuawa ili zipatikane pesa za kutusaidia !
Kama masuala haya pia yatakuwa agenda kwenye mkutano huo basi bara la Afrika litakuwa limetendewa haki ya kweli.
Tuesday, November 07, 2006
Subscribe to:
Posts (Atom)