Wednesday, October 05, 2005

Samahani

Nimejaribu kualika watu pasipo na viti, samahani nilisahau, nafasi za watu kukaa. Walikuja wengi sana wakakuta hakuna nafasi ya kukaa hata mtu mmoja, sijui kama waliondoka kimyakimya kama mchungaji anaposisitiza watu wachangie sadaka nyingi zaidi au walitukana kama siku yanga ilipofungwa na simba.
Unajua kila kitu kina aina yake, kama vile wengine huandaa tafrija ndipo waalike watu kusheherekea kwa kunywa na kula lakini wengi hualika watu kuja kusaidia kuandaa tafrija hata kama haiwahusu au haina ulazima kwao wanatakiwa "kuchangia" ili ifanikiwe. Samahani hivi mimi ninaonekana niko kwenye kundi lipi?
Habari huandikwa na mwandishi wa habari lakini mimi sio mwandishi wa habari wa kuandikia watu, nataka watu waniandikie mimi nizisome habari zao, mko tayari kuniandikia bila malipo? Je watu hupenda kusoma kila habari iliyopo, sijui kama ukimwanbia Rasta afrika siyo kwao atakusadiki, labda ukitumia njia nyingine ambayo sijawahi kuisikia .
Habari zipo nyingine ni nzuri na nyingine ni mbovu nani anajua habari iliyo nzuri kila wakati, kama ni hivyo waandishi wasingekuwa wanazeeka na kujiuzulu kila siku au kufukuzwa kazi kwa ufanisi mbovu.Sio kama sikubaliani na uwapo wao, ila nahitaji kuwa na busara zaidi ya ile ipatikanayo toka kwa mmoja mmoja.
Kaa tuongee nilikuta nyumba ya wageni moja pale livingstone nchini zambia inaitwa tulye tonje nikaambiwa maana yake ni kaa tuongee, sijui kama itakuwa na uhusiano na hii kaa tuongee, hapa panaendeleza na hatufanyi mambo ambayo yatamdhuru mtu, sikumbuki kilichokuwa kinafanyika tulye tonje, maana nilifika usiku na mchovu wa safari hivyo nilifurahia kupata kitanda kama nimefika safari yangu.
Karibuni tukae tuongee, kila mmoja ashiriki katika maongezi haya tupate kilicho kweli hata kama kitawauma wengi na wachache wengine wajue kwamba wamekalia misumari na wasiponyanyuka haraka itawachoma washindwe kukaa kesho kama kesho huwa inafika.

2 comments:

mwandani said...

Nafasi i wazi, vipepeo hurutubisha kila ua - vipepeo nasi tumo.
Mafahali humiliki kwa nguvu - wenye kauli za nguvu nasi tumo.
Mabata huchokora-chokora , husambaza tope, na kuharibu mimea,
mabata nasi tumo. Ndio utamu wa 'open space' Si utamaduni mgeni, teknolojia tu. Zamani wazee walikaa mduara wwakiota moto na kuongea, mwenye kuchangia kwa mazuri kama kipepeo alichangia, aliyetifua kama bata...
Karibu Mloyi

mark msaki said...

nashukuru kaka mloyi!

nimefika na nimepata jamvi! hala hala tuanze kulitandika gumzo! hata kama likachanika sio mwisho ya mazungumzo! maneno huumba maneno huua, nashukuru mwenyezi sisi hapa tunaumba! naam si kuumba tu huu ni mtambo wa kurekebisha maadili!

karibu sana!