Tuesday, November 07, 2006

Kikwete uso kwa uso na Al-Bashir

Wakati viongozi wa Afrika wanakutana na wenzao wa Uchina huko Beijing, China kuna mikutano mingine ya chini chini inaendelea baina ya viongozi wa nchi za kiafrika wanaohudhuria Mkutano huo mkubwa unaotarajiwa kulipatia manufaa makubwa sana bara la Afrika.
Uchina huwa haiamrishwi na Marekani na rafiki zake washirikiane na nani, hivyo maadui wakubwa wa jamii ya Marekani nao pia watahudhuria Mkutano huo mkubwa ambavyo Vyombo vya Habari(uongo!) wameanza kuutilia shaka bila ya kuwa na shaka na mambo yao wenyewe. Viongozi wa Afrika walioalikwa yumo kinara wa Afrika Raisi Bob Mugabe wa Zimbabwe aliye kwenye orodha kuu ya maadui wa magharibi, pamoja na Raisi wa Sudani Bwana Al-Bashir ambaye anasahau uafrika wake na kubariki kuangamizwa wenzake wa jimbo la Durfur kwa Sababu wao ni weusi zaidi yao! Na nywele zao ni ngumu sana!
Bila shaka, lazima Raisi wetu Mhe. J Kikwete na wenzake wengine watapata wasaha wa kukutana na Bw. Al-Bashir, na kufanya mazungumzo yaliyo au yasiyo rasmi. Ingawa kuna mambo mengi sana ya kuongelea ikiwamo ruhusa ya Tanzania kutumia maji ya Ziwa Nyanza! kukaribisha wawekezaji toka Sudan, uhusiano baina ya nchi hizi mbili. Ila bila kuongelea na ikibidi kukemea tabia au kusudi la Bw. Al-Bashir la kufumbia macho mauaji ya Durfur atakuwa hajawatendea haki watanzania na waafrika wote kwa ujumla, pia atakuwa hajatekeleza kipengele cha ilani yake ya uchaguzi aliyokuwa ameikariri kuliko misahafu kipindi cha kampeni cha kushughulikia migogoro ya jirani zetu.
Sitegemei kama kuna Mtanzania anayeunga mkono mauuaji hayo yanayoendelea kwa kasi sana, huku serikali ya sudan ikitajwa kuliimarisha jeshi la wauaji kwa kuwapatia silaha na kuzuia jeshi la nje kuingilia kati mauaji hayo.
Hivyohivyo, ingawa China ametuita kutupatia msaada naye inabidi aambiwe kwamba soko lake la silaha la Sudani linatuumiza sana kuliko hiyo misaada anayotaka kutupatia hivyo aache kuwauzia silaha wasudani na kwanza aingilie hayo mauaji ya Durfur na kuhakikisha yanakoma la siyo hiyo misaada yake haitakuwa na maana kwetu na itatuchefua zaidi kuona waafrika wanazidi kuuawa ili zipatikane pesa za kutusaidia !
Kama masuala haya pia yatakuwa agenda kwenye mkutano huo basi bara la Afrika litakuwa limetendewa haki ya kweli.

Friday, September 15, 2006

Ya Mugabe yamekemewa haya jee?

Nadhani ni wachache sana wanaojua kisiwa kinachoitwa chagos, kisiwa hiki kipo karibu na Tanzania kwenye bahari ya hindi na zaidi vipo karibu na visiwa vya mauritius. na wakazi wake ni waafrika weusi na matabaka mengine.
Kumbuka Ulimwengu wa Magharibi ukiongozwa na uingereza, Australia na Marekani wanavyompigia kelele na vitimbi vya kila aina shujaa wetu Bob Mugabe kwa kuwanyang'anya/ kuwapunguzia ardhi wazungu wachache pale Zimbabwe waliokuwa wamejilimbikizia ardhi huku weusi wengi wakiwa hawana ardhi hata za kujenga vibanda vya kuishi na familia zao.
Nimekuta katika jarida la New African toleo la Agosti/september 2006 Habari inayosikitisha na kuwaumbua hao kuwa wanachotaka Zimbabwe sio demokrasia wanayoisemwa ila kuna jingine lililojificha. Katika kipindi cha miaka ya 1965, na 1973 wakazi zaidi ya 2,000 wenyeji wa visiwa hivyo walifukuzwa toka kwenye visiwa hivyo na Uingereza na Marekani wakihamishiwa uhamishoni kwenye visiwa vya mauritius na shelisheli ili visiwa vyao vitumike kama vituo vya kijeshi vya Uingereza na Marekani na pia kwa utalii.
Wenyeji wa visiwa vya Chagos hawakukubaliana na uamuzi huo wakaendesha kampeni ,toka siku hizo mpaka leo bado wanaendelea, katika kesi iliyohukumiwa na mahakama kuu ya uingereza na mheshimiwa jaji Cresswell na Jaji Hooper kuwa uamuzi wa kuwafukuza haukuwa na busara na unachukiza wao, serikali ya Uingereza wanaukataa na kung'ang'ania kukata rufaa juu ya hukumu hiyo huku wakishinikizwa na rafiki zao Marekani kwa kuhofia usalama iwapo wa-chago watarejea kwenye ardhi yao ya asili.
Najaribu kufananisha hizi hali mbili; chagos na zimbabwe bila kupata jibu, ila nimeona kuwa hii ni vita nyingine ya kukomboa sehemu nyingine ya bara la afrika iliyosahaulika na ambayo hakuna anyeitangaza.

Saturday, August 19, 2006

Maamuzi na Maazimio

Unafanya maamuzi na kuyatimiza!
Unaamua nitakuwa nakula mara moja kwa siku ili niushinde ugonjwa wa "obesity" unafanya hivyo mpoka unazoea na 'obesity' haiwi tena tatizo la kusumbua akili yako.
Unaamua kuwa kibaraka, unakuwa na kutajirika kwa gharama ya waliokuwa wazalendo wenzako.
Unaamua kuwa wa dini hii, na unakuwa.
Unaamua kutovaa viatu kwa sababu zako na unaacha kuvaa viatu kama alivyofanya Mutabaruka.
Hata kama huwezi kuwaeleza wengine wakubaliane na maamuzi yako lakini hayo ndiyo maamuzi yako mwenyewe na unaamini yanamanufaa kwako.
Tatizo kubwa ni pale unapofanya maamuzi yako na kuyatekeleza kwa gharama za wenzako na bila ridhaa yao hata kama watayakubali kwa kuburuzwa ndipo yanakuwa sio maamuzi mazuri.
Wiki chache zilizopita Dunia ilikuwa kwenye kilio kikubwa kutokana na vita ya Hamas Na Israeli, ingawa sasa mapigano kwa kiwango kikubwa sana tunasema yamesimamiswa lakini inabidi tuliangalie suala hilo sasa, nini kilileta mapigano hayo? Ardhi ya waarabu, uchokozi wa Hamas, au ubabe wa waIsraeli? Hakukuwa na njia nyingine ya kufuata kutatua matatizo hayo zaidi ya kusababisha mauaji ya maelfu ya watu? majibu ni mengi kuliko maswali.
Ukiamua kujenga nyumba yako mabondeni mimi hainihusu mradi tu usizibe ule mto ufanye kipindi cha masika maji yafurike mpaka nyumbani kwangu.
Hawajama walioamua kuwa 'mateja' haituhusu kama hawatatuingilia, tunapiga kelele sababu hawana njia nyingine ya kupata pesa kwa ajili ya hiyo starehe yao zaidi ya kuvunja nyumba zetu, kutuchomolea mifukoni kutukaba na hata kutudhuru hadi kifo, kama watakuwa na njia nyingine za kutimiza strehe zao nadhani tusingejali sana ilimradi hawakai kwenye mapito yetu kama takataka(kwa uchafu) zinazosubiri kupelekwa dampo na kutubughudhi.
Ukiamua kuwa masikini asiye na malengo hakuna atakayekuingilia, ila wanasiasa fulani watatumia hali yako kujipatia umaarufu kama hutakuwa thabiti kwenye maamuzi yako.
Mtoto akiamua asipende kusoma kwa sheria za sasa mwalimu hatahangaika kumfuatafuata, jua hakielimu wanapigia debe walimu wasiruhusiwe kuchapa viboko bila kutoa njia mbadala kwa mazingira ya Tanzania, akiogopa sheria na kujua mwisho wa mwezi mshahara ni uleule wa kutumia wiki mbili aanze tena kukopakopa.
Ukiamua kuwa hivi kuwa mradi huwaingizi wengine kwenye maamuzi yako na wengine wanatakiwa kuwapa nafasi wenzao kuwa wanavyotaka kama anavyofanya mungu kwa kuwapa nafasi sawa watu wote.

Wednesday, June 21, 2006

Afrika inathaminiwa vipi na ....

Wakati sisi tunawaza kwenda ughaibuni kutafuta maisha kuna wengine wanalilia kuja Afrika kutafuta maisha na kuishi, watu hawa wana sababu za msingi kuhusu uamuzi wao wa kuja kuishi na kuendesha maisha yao Afrika. Wimbi hilo la watu kuja kuishi afrika linaendelea hadi kwa waafrika wenzetu wanaoishi uhamishoni. Ingawa inakuwa vigumu kidogo kwao kuchagua mahali pa kuhamia lakini hawa wameshafanya uamuzi wao au wako njiani

Tuesday, May 23, 2006

Mkaribisheni mgeni.

Kamala Godwin amependezewa na blogu zinavyofanya kazi, ameamua kujiunga kwenye mtandao huu, yeye anapatikana hapa mtembeleeni.
Hawa wameumbwaje?

Burning Spear aliuliza hivi, ….Unakumbuka siku za utumwa? Babu zetu walivyochukuliwa kama vifaa vya kufanyia kazi. Wengine wengi mpaka leo wanahoji hivi utumwa ulikuwa halali? Maswali huwa hayaishii hapo tuu, mengine mengi hufuatia kama vile ukiwa Afrika na makazi ya waafrika kote duniani utasikia maneno haya …..Unajua hawa watu wa ulaya wanatunyonya sana! Ukiwa kwenye maeneo ya wazungu ukikutana na waafrika wengi wao watakwambia Unasikia bwana hapa tatizo kubwa ni kubaguliwa, tunachukuliwa sisi (waafrika) kama watu wa daraja la chini sana … Ukikuta maraisi wa Afrika kwenye mkutano wataongelea tofauti katika mgao wa biashara baina ya nchi za Afrika na za magharibi( Ulaya na Marekani) hawa hujadili njia madhubuti ya kuleta usawa na kuzinufaisha nchi za kiafrika katika biashara ya dunia.
Dunia nzima na sasa hata watoto wao wazungu sasa wameanza kuwasema baba, mama, babu na bibi zao kwa wanachowafanyia waafrika na wa-Asia kiasi cha kujitolea maisha yao kupambana na Dola zao. Lakini wengi wao hawatajibu au kufanya lolote kuhusu jambo hilo na wala hawatachukia maneno yako wala kuyafurahia.
Ukimsikiliza Tony Blair , Joji Kichaka na wengine wa aina hiyo watakubali machono mwako kwamba waafrika wanadhulumiwa na kuna haja ya kufanya mabadiliko ili kubadili mfumo uliopo sasa na kuahidi kutoa kipaumbale kwa jambo hilo.
Wataunda kamati za kushughulikia jambo hilo lakini matokeo yake yatakuwa labda hawataongelea tena matokeo ya kamati hiyo au ufumbuzi utakaotolewa utaleta matatizo na manung’uniko mengi zaidi!
Cha kushangaza ni uvumilivu wa wazungu kuhusu kauli zinazowakosoa na manung’uniko wanayopata kutokana na matendo wanayowafanyia watu wa asili nyingine tofauti na zao. Nashindwa kuelewa uumbwaji wao ulikuwa wa aina gani kwani sisi waafrika tukisemwa kidogo huwa tunajirekebisha na kufuata ushauri tuliopewa na “wenzetu”.

AU, NEPAD NA Viongozi

Nimesoma mawazo haya kwenye NewAfrikan na kushangaa kweli kuhusu ukweli wa saga la Charles Taylor. Sijui huku kugeukana kutaisha lini!. Bonyeza hapa usome na mimi.

Thursday, May 18, 2006

Unawasikiliza hawa?






Ndesanjo ametuwekea kiunganishi kwenda kwa baadhi ya watu hawa lakini sidhani kama huwa tunajaribu kuwapitia. Hawa ni washairi wa ki-reggae wanachanganya usomaji wa mashairi na midundo ya reggae katika hali fulani ambayo inapendezesha sana mashairi yao.

Kushoto kabisa anaitwa Michael Smith yeye habari zake nyingi hazijulikani sana lakini niliwahi kupata kazi yake moja kwenye shairi la 'me cyant believe it' na lingine ambalo sikumbuki jina lake. Inasemekana kutokana na msimamo wake dhidi ya chama kilichokuwa kinatawala na ukali wa maneno yake wafuasi wa chama tawala kule Jamaika walimvamia akiwa sokoni na kumponda mawe mpaka mauti yalupompata.

Hizo mbili za katikati ni Mutabaruka maarufu kwa mashairi ya ukombozi, Yeye habari zake zipo kwenye kiunganishi katika jina lake. Nakumbuka alipohojiwa kwenye muhutasari wa maisha ya Peter Tosh alisema kwamba... unapodai haki yako huhitaji kujadiliana na mdaiwa wako maana unakuwa unaipoteza haki yako..... na katika mahojiano mengine alisema ..... Afrika inasubiri waumbaji wake.... Jaribu kumfuatilia.

Picaha ya mwisho wako wawili, kushoto ni Benjamin Zephaniah, maarufu kwa mashairi na mweusi ambaye alikataa tuzo ya OBE aliyopewa na Malkia lizabeth, rudia siku Beckham alipopewa tuzo hiyo, kwa madai malkia hawajali waafrika ili anajikomba kwake. Kulia ni Linton Kwesi Johnson, aliyeshangilia upinzani dhidi ya ubaguzi wa weusi uingereza, katika shairi hilo alisikika akisema, .... kidonge cha ukandamizwaji kilitapikwa na polisi wawili walikufa..... kama ishara ya ushindi dhidi ya ubaguzi.

Wote wanne ni wazaliwa wa Jamaika .Mutabaruka yeye anaishi Jamaika, Kwesi na Benjamin Zephaniah wanaishi uingereza.

Tuesday, May 16, 2006

Miaka 25 ya kifo cha Bob Marley...

Wiki iliyopita kulikuwa na sherehe na matamasha ya kumkumbuka gwiji la reggae Bob Marley, kama anavyojulikana na wengi,
mwingine alifanya kumbukumbu hiyo kwa njia nyingine, Huyu sio mwingine bali ni rafiki wa karibu sana wa Bob Marley na mpiga gitaa wake maarufu Aston Barret au "Family man". Kumbukumbu yake ilikuwa ni kukumbuka jinsi alivyosaidiana na Bob na wengine wanavyofaidika siku hizi na yeye na ndungu wa marehemu mdogo wake walivyoachwa masikini bila kukumbukwa, madai yaliyomfanya afungue kesi mahakamani na nakala ya hukumu yake
hii hapa .

Thursday, May 04, 2006

Moto moto moto kila mahali ....

Nimejaribukuweka tena viunganishi nilivyokuwa nimekosea kama mlivyonishauri na sasa viko fiti kwa kufanyiwa tizi. Angalia nakala iliyopita ya blogu kila mahali ujionee ilivyo.
Picha pia zimeanza kuonekana unaweza kuona nyingi zaidi kwenye flickr Lakini hii isimtishe Michuzi kwamba staili yake imeingiliwa na kupikuliwa, bali imehamasisha blogu nyingine zaidi. sijui Mpoki Bukuku alihamasishwa kwa muda tuu!( just a passing glance) Motowaka hata "share a moment" na michuzi ataishi pale.

Ingawa sasa nimebadilika kidogo, Hii ilikuwa Mwaka 2003 Nilipokuwa picha ya kwanza Capetown na ya pili kwenye basi Livingstone, Zambia. Bado najilaumu kwa kutopiga picha nyingi na nzuri kuliko hizi.

Wednesday, March 29, 2006

Vibaraza vinaendelea.....

Vibaraza bado vinaendelea, kuna kipya cha Simba na Yanga lakini mwenyewe hasemi kama ni Simba au Yanga ,mimi naona kakaa kama Yanga vile,
Mtembelee hapa. Umuulize yeye ni simba au yanga, asipojibu shauri yake.
Mwandani sasa ameweka picha yake lakini sio mojakwamoja kama humjui huwezi kujua ni nani yule, lakini binti Simba anatuambia
huyu ni mwandani. Hilo afro bado lipo kama siku tulipoachana Tambaza Boys sekondari.
Yule mnakala maarufu wa mwananchi, Yahya cherehani na yeye pia ameingia kwenye blog,Naona sasa blog zinateka watu wote waume kwa wake wenye habari motomoto. Yeye
anashona kuliko cherehani ya mchina bila kutia umbeya na uwongo wa wanasiasa.
Ndesanjo naye kwenye nyumba yake mpya mambo bado ni moto sana.
Angalia kesho vibaraza vitakuwa vipi.

Friday, February 24, 2006

Bado nipo..

Sio kama nimeondoka kimyakimya bado nipo ila mambo yaliingiliana kidogo ndiyo maana niko kimya. Wordpress imekuja kwa kishindo kama ilivyokuja Blogspot inatamanisha kuhamia kwenye hayo makazi mapya, bado ninafikiria kama yatakuwa mapya siku zote au ndiyo kilekile, kipya kinyemi na kuwa wa kileo hata kama hujafika leo!
Ndio ninapata matatizo kidogo kutumia blogspot, mpaka leo sijaweka picha yangu hapa,labda nimezoea "cut and Paste" iliyorahisi bila kuzungukia njia nyingine, lakini hapa tunapendana zaidi kupaacha sio rahisini kama kukubali kufa na kuwaacha uwapendao dunuani.
Mijadala inazidi kupanuka, kila kitu kinawekwa wazi hapa. Kuna kusanyiko la waandishi wa habari, wasomaji wa habari wanaopenda kugawia wenzao habari walizoziona kwenye sehemu mbalimbali, watu wa soga, watuma picha na wa udaku pia. Wanablogu wa kiswahili tumeungana kwa kiasi kikubwa, sote tunashirikiana na kujuana kwa majina ingawa hatujuani kwa sura, siwezi kusema kwamba hakuna wanablogu wa kiswahili walionje ya mtandao huu.
Blogu nyingi zimevuma hapa wakati kama hii yangu inatokea kwa nadra na bila viunganishi motomoto, ukitaka viunganishi motomoto unaweza kupitia makene, ndesanjo , Nambidza na kuzunguka kwenye blogu zote za kiswahili zilizo kwenye mtandao huu.
Ushirikiano na kutembeleana kati yetu tuuendeleze, tusiwaache wenzetu waliohapa maana wametueleza walipohamia hivyo bado tupo nao, tuwatembeleeni ili tuendelee kufaidika na mawazo na ufahamu wao.

Tuesday, January 10, 2006

Salaam ndugu...., habari za nyumbani? watoto?

Fikiria maisha yatakuwaje iwapo pale utokako nyumbani asubuhi kila uingiapo salamu zitafuata mlolongo huu.

Uingiapo kwenye Daladala unaanza kumsalimia mpiga debe ndugu habari za kuamka, nyumbani hawajambo, mama? watoto? halafu unahamia kwa konda, Habari gani? Vipi kazi leo? imeanza vizuri? mbona unaonyesho uchovu asubuhi hii yote? hukulala nini?. Naye konda anaanza kupita kwa kila mtu habari kaka/dada, Leo umechelewa kutoka? au mabasi ya shida leo? poleni sana, naomba nauli.

Mwendo unakuwa huu huu kwa kila unayekutana nae siku hiyo muuza chai, muuza machungwa,walinzi, makarani wa benki, watu wanaofanya promosheni maofisini na ndugu zao machinga, bila kusahau unaingia kwenye blogu zote unaweka salamu za asubuhi kwa kila moja.

Fikiria tena utatumia muda kiasi gani kutoa hizo salamu zote! utakuwa katika hali gani? utaweza kuendelea na kazi siku hiyo? Kazi ngapi zitasimama? foleni itakuwa kubwa kiasi gani?.

hivyo ndiya watu wanavyotaka iwe siku yao na wewe pia uwaige .